Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.23 Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.24
Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu. 15
Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo. 26