Uislamu umelingania katika kusimamisha uadilifu kati ya watu na pia uadilifu katika vipimo vya ujazo na uzito
Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa Yeye. Imekwisha kufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.85
Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. 8
Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo kuwaidhini Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona. 58
Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani,na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka. 90
Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka. 27
Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda. 28
Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda. 6
Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalo dhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki. 9
Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe. 10
Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu. 11
Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu. 12
Mtume swala na salamu zimuendee amesema: hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake analolipenda. Amepokea Muslim.