Jawabu: Suratul Humaza na tafsiri yake:
Naanza kusoma Qur’an kwa jina la Mwenyezi Mungu nikiomba msaada Wake. «Allah» ni jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa baraka Mwenye kutukuka, Anayestahiki kuabudiwa na sio mwingine. Nalo ni jina mahsusi zaidi miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na haitwi kwa jina hili yeyote isipokuwa Yeye Aliyetakasika na sifa za upungufu. «Al-Raḥmān» Mwenye rehema nyingi Ambaye rehema Zake zimewanea viumbe vyote. «Al-Raḥīm» mwenye kuwarehemu Waumini. Na majina mawili haya, kati ya majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, yanakusanya uthibitishaji wa sifa ya urehemefu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kama unavyonasibiana na haiba Yake.
"Shari na maangamivu yatampata kila mwenye kusengenya watu na kuwatukana." "Ambaye hamu yake ni kukusanya mali na kuyahesabu." "Akidhani kuwa mali yake ambayo ameikusanya itampa dhamana ya kuishi milele duniani na kukwepa kuhesabiwa." "Anavyodhania sivyo. Atatiwa ndani ya Moto ambao huvunjavunja kila kinachotiwa." "Ni kipi kinachokujuza ni kipi kinachovunja vunja?" "Huo ni Moto wa Mwenyezi Mungu uliowashwa." "Ambao kwa ukali wake hupenyeza miilini ukafikia kwenye nyoyo." "Moto huo umefungiwa juu yao wakiwa wametiwa minyororo" "Na pingu ndefu ili wasitoke." [Suratul Humaza: 1-9]
Tafsiri:
"Shari na maangamivu yatampata kila mwenye kusengenya watu na kuwatukana." Tatizo kubwa na adhabu kali kwa mtu anayewasengenya watu kwa wingi, na kuwasema vibaya.
"Ambaye hamu yake ni kukusanya mali na kuyahesabu.": Ambaye pupa yake ni kukusanya mali na kuzihesabu, hana malengo mengine zaidi ya hayo.
"Akidhani kuwa mali yake ambayo ameikusanya itampa dhamana ya kuishi milele duniani na kukwepa kuhesabiwa." Anadhani kuwa mali yake aliyoikusanya itamuokoa na mauti, kuwa atabakia milele katika maisha ya dunia.
"Anavyodhania sivyo. Atatiwa ndani ya Moto ambao huvunjavunja kila kinachotiwa." Uhakika si kama anavyofikiria huyu mjinga, Hakika atatupwa katika moto wa Jahanam ambao unagonga na kukivunja kila kinachorushwa ndani yake kwa ukubwa wa ugumu wake.
"Ni kipi kinachokujuza ni kipi kinachovunja vunja?" Na ni kipi kilichokufahamisha ewe Mtume ni upi moto huu ambao unavunjavunja kila kinachotupwa ndani yake?!
"Huo ni Moto wa Mwenyezi Mungu uliowashwa." Huo ni moto wa Mwenyezi Mungu uliochochewa.
"Ambao kwa ukali wake hupenyeza miilini ukafikia kwenye nyoyo." Ambao unapenyeza katika mili ya watu na kufika mpaka katika nyoyo zao.
"Moto huo umefungiwa juu yao wakiwa wametiwa minyororo" Hakika moto huo umefungwa juu ya wale wenye kuadhibiwa ndani yake.
"na pingu ndefu ili wasitoke." Kwa nguzo imara ndefu ili wasiweze kutoka ndani yake.