Jawabu: Suratut Falaq na tafsiri yake:
Naanza kusoma Qur’an kwa jina la Mwenyezi Mungu nikiomba msaada Wake. «Allah» ni jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa baraka Mwenye kutukuka, Anayestahiki kuabudiwa na sio mwingine. Nalo ni jina mahsusi zaidi miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na haitwi kwa jina hili yeyote isipokuwa Yeye Aliyetakasika na sifa za upungufu. «Al-Raḥmān» Mwenye rehema nyingi Ambaye rehema Zake zimewanea viumbe vyote. «Al-Raḥīm» mwenye kuwarehemu Waumini. Na majina mawili haya, kati ya majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, yanakusanya uthibitishaji wa sifa ya urehemefu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kama unavyonasibiana na haiba Yake.
Sema «Najilinda kwa mola wa mapambazuko". «Kutokana na shari la viumbe na udhia wao" «Na shari ya usiku wenye giza jingi uingiapo na ujikitapo na shari na maudhi mbalimbali yaliyomo ndani yake." «Na shari ya wachawi wenye kupuliza kwenye mafundo wanayoyafunga kwa lengo la kuroga." «Na shari ya hasidi mwenye kuchukia watu, anapowahusudu na kuwadhuru, kwa kutaka neema za Mwenyezi Mungu Alizowaneemesha ziwaondokee.» [Suratul Falaq: 1-5].
Tafsiri:
Sema «Najilinda kwa mola wa mapambazuko". Sema ewe Mtume- Najikabidhi kwa Mola muumba wa asubuhi, na ninajiweka karibu kwake.
"Kutokana na shari ya vile alivyoumba": Kutokana na shari ya vile vyenye kuudhi katika viumbe vyake.
«Na shari ya usiku wenye giza jingi uingiapo na ujikitapo na shari na maudhi mbalimbali yaliyomo ndani yake.": Najikabidhi kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shari ambazo zinajitokeza usiku miongoni mwa wanyama na wezi.
«Na shari ya wachawi wenye kupuliza kwenye mafundo wanayoyafunga kwa lengo la kuroga.": Na ninajikabidhi kwake kutokana na shari za wanga ambao hupuliza katika mafundo wanaporoga.
«Na shari ya hasidi mwenye kuchukia watu, anapowahusudu na kuwadhuru, kwa kutaka neema za Mwenyezi Mungu Alizowaneemesha ziwaondokee.» Na kutokana na shari za hasidi mwenye kuwachukia watu anapowahusudu juu ya yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika neema, akitaka ziwaondokee, na kuwatia maudhi.