Sehemu ya Hadithi:

Jawabu: Kutoka kwa kiongozi wa waumini Abuu Hafsi Omari bin Khattwab Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: Nilimsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu Rehema na Amani ziwe juu yake akisema: "Hakika matendo yote huzingatiwa nia, na hakika kila mtu hulipwa kwa lile alilolinuia, atakayekuwa kuhama kwake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi (malipo yake yatakuwa) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na atakayekuwa kuhama kwake ni kwa ajili ya dunia ataipata, au kwa ajili ya mwanamke ili amuoe, basi kuhama kwake kutakuwa ni kwa lile alilolihamia". Ameipokea Bukhari na Muslim.

Faida zinazo patikana katika hadithi

1- Kila matendo lazima yawe na nia, kama swala, na swaumu, na Hijja, na matendo mengine.

2- Ni lazima kutakasa nia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hadithi ya pili:

Jawabu: Kutoka kwa mama wa waumini mama Abdillah Aisha Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: amesema Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili (Dini yetu hii) jambo ambalo si katika dini hii basi atarejeshewa jambo hilo alilolizua" Ameipokea Bukhari na Muslim.

Faida zinazo patikana katika hadithi

1- Katazo la kuzua katika dini.

2- Na yakwamba matendo yote yenye kuzushwa hurejeshwa na hayakubaliki.

Hadithi ya tatu:

Jawabu: Kutoka kwa Omar Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake Amesema: "Tukiwa sisi tumekaa kwa Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- siku moja, ghafla akatokeza mwanaume mmoja, mwenye nguo nyeupe sana, mwenye nywele nyeusi sana, hazionekani kwake athari za safari, na wala hakuna anayemfahamu yeyote katika sisi, mpaka akakaa kwa Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake akashikanisha magoti yake na magoti mtume Rehema na Amani ziwe juu yake (mfano wa kikao cha tahiyatu) na akaweka mikono yake juu ya mapaja yake, Na akasema: Ewe Muhammadi, nieleze kuhusu Uislamu? Akasema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani ziwe juu yake: Uislamu ni kushuhudia kuwa hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa ni Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammadi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na udumishe swala na utoe zaka, na ufunge Ramadhani, na uhiji nyumba tukufu ukipata uwezo wa kuifikia, Yule bwana akasema: "Swadakta"-Yaani: Umesema kweli, Tukamshangaa! Anamuuliza na anamsadikisha! Akasema: Nieleze kuhusu Imani? Akasema: Ni kumuamini Mwenyezi Mungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume wake na siku ya mwisho, na uamini makadirio kheri yake na shari yake, Akasema: "Swadakta"-Yaani: Umesema kweli, Basi hebu nieleze kuhusu Ihsani (wema)? Akasema: Ni umuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba wewe unamuona, na kama wewe humuoni basi yeye anakuona: Akasema: Hebu nieleze kuhusu kiyama: Akasema: hakuwa muulizwaji kuhusu hilo ni mjuzi kuliko muulizaji, Akasema: Hebu nieleze kuhusu dalili zake? Akasema: ni mjakazi kuzaa bwana wake, na ukawaona watembea peku,uchi na masikini wachunga mifugo wakishindana kujenga majengo marefu, kisha yule bwana akaondoka, akakaa muda kidogo kisha akasema: Ewe Omari unamjua ni nani huyo muulizaji? Nikasema: Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuzi, Akasema: Basi bila shaka huyo ni Jibril alikuja ili akufundisheni dini yenu". Imepokelewa na Imamu Muslim

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Kumetajwa ndani yake nguzo tano za uislamu; nazo ni:

1- Ni kushuhudia kuwa hapana mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake na muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.

2- Na kudumisha swala.

3- Na kutoa zaka.

4- Kufunga ramadhani.

5- Na kuhiji nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu.

2- kumetajwa nguzo za imani, nazo ni sita:

Kumuamini Mwenyezi Mungu.

Na Malaika wake.

Na vitabu vyake.

Na Mitume wake.

Na siku ya mwisho.

6- Na makadirio kheri yake na shari yake.

3- Kumetajwa nguzo za ihsan, nayo ni nguzo moja, nayo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu kama unamuona, na ikiwa wewe humuoni basi yeye anakuona.

4- Wakati wa kusimama kiyama, hakuna aujuaye isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hadithi ya nne:

Jawabu: Kutoka kwa Abuu Huraira Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: amesema: Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake: "Muumini aliyekamilika kiimani ni yule mwenye tabia nzuri zaidi kuliko wengine". Kaipokea Tirmidhiy na akasema: Hadithi ni nzuri na ni sahihi".

Faida zinazo patikana katika hadithi

1- Himizo la kuwa na tabia njema.

2- Na yakwamba ukamilifu wa tabia ni katika ukamilifu wa imani.

3- Na yakwamba imani inaongezeka na kupungua.

Hadithi ya tano:

Jawabu: Kutoka kwa Abdallah bin Omari Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao, ya kwamba Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake amesema: "Mwenye kumuapia asiyekuwa Allah atakuwa amekufuru au kamshirikisha Allah." Kaipokea Imamu Tirmidhiy

Faida zinazo patikana katika hadithi

-Hafai kuapa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

- Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni katika shirki ndogo.

Hadithi ya sita:

Jawabu: Kutoka kwa Anasi Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake: "Hawezi kuamini mmoja wenu mpaka niwe napendeka zaidi kwake kuliko mtoto wake, mzazi wake, na watu wote." Ameipokea Bukhari na Muslim.

Faida zinazo patikana katika hadithi:

- Kumpenda Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake ni wajibu kuliko mapenzi ya watu wote.

- Na yakwamba hilo ni katika ukamilifu wa imani.

Hadithi ya saba:

Jawabu: Kutoka kwa Anasi Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake: "Hawezi kuwa na imani mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake anachokipenda yeye katika nafsi yake" Ameipokea Bukhari na Muslim.

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Ni juu ya muumini kuwapendelea waumini kheri kama anavyoipendelea nafsi yake.

- Na hilo ni katika ukamilifu wa imani.

Hadithi ya nane:

Jawabu: Kutoka kwa Abuu Saidi Al Khudry Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kutoka kwa Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake amesema: "Namuapia yule ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake! Hakika hiyo inalingana na theluthi ya Qur'ani" Imepokelewa na Al-Bukhaariy

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Ubora wa suratul Ikhlaswi.

2- Nakwamba sura hiyo inalingana na theluthi ya Qur'ani.

Hadithi ya tisa:

Jawabu: Kutoka kwa Abuu Mussa Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake: "Neno 'Laa haulaa walaa quwwata illaa billaah' Hakuna ujanja wala nguvu isipokuwa zinatoka kwa Mwenyezi Mungu, ni hazina miongoni mwa hazina za pepo" Ameipokea Bukhari na Muslim.

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Ubora wa neno hili, nakwamba neno hili ni hazina miongoni mwa hazina za pepo.

2- Linamuweka mbali mja na ujanja wake na nguvu zake, na kutegemea kwake kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake.

Hadithi ya kumi:

Jawabu: Kutoka kwa Nuaim bin Bashiri Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: Nilimsikia Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake akisema: "Tambueni kuwa hakika katika kiwiliwili kuna kipande cha nyama kitakapotengemaa mwili mzima unatengemaa, na kikiharibika mwili mzima una haribika, tambueni, kipande hicho ni moyo" Ameipokea Bukhari na Muslim.

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Kutengemaa kwa moyo ndani yake kunapelekea kutengemaa kwa mtu nje na ndani.

2- Kutilia umuhimu kurekebisha moyo, kwa sababu moyo ndiyo unaomfanya mtu atengemae.

Hadithi ya kumi na moja:

Jawabu: Kutoka kwa Muadh bin Jabal Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, Amesema: Amesema Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake: "Yatakayekuwa maneno yake ya mwisho duniani ni: Laa ilaaha illa llaah- Hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu ataingia Peponi". Imepokelewa na Abuu Daud

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Ubora wa neno, Laa ilaaha illa llaahu, nakwamba mja ataingia peponi kwa neno hilo.

2- Na ubora wa mtu ambaye yatakuwa maneno yake ya mwisho kutoka duniani ni Laa ilaaha illa llaahu.

Hadithi ya kumi na mbili:

Jawabu: Kutoka kwa Abdilah bin Masoud Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, Amesema: Amesema Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake: "Muumini si msemaji watu vibaya, wala mtoaji wa laana, wala muovu, wala mwenye kauli chafu" Kaipokea Imamu Tirmidhiy

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Katazo la maneno yote ya batili na machafu.

-Na yakwamba hiyo ndiyo sifa ya muumini katika ulimi wake.

Hadithi ya kumi na tatu:

Jawabu: Kutoka kwa Abuu Huraira Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: amesema: Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake: "Katika uzuri wa uislamu wa mtu: Ni kuacha kwake yale yasiyomuhusu" Kaipokea Tirmidhiy.

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Mtu kuyacha yasiyomuhusu katika mambo ya dini ya mtu mwingine au dunia yake.

2- Kuacha yasiyomuhusu ni katika ukamilifu wa uislamu wake.

Hadithi ya kumi na nne:

Jawabu: Kutoka kwa Abdillah bin Masoud: Yakwamba Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake, amesema: "Atakayesoma herufi moja katika kitabu cha Mwenyezi Mungu basi atapata jema moja kwa herufi hiyo, na jema moja hulipwa mara kumi mfano wake, sisemi: Alif Laam Miim ni herufi moja, Lakini, alifu ni herufi, na Laam ni herufi, na Miim ni herufi" Kaipokea Imamu Tirmidhiy

Faida zinazo patikana katika hadithi:

1- Ubora wa kusoma Qur'ani.

2- Na yakwamba kwa kila herufi unayoisoma unapata mema mengi kwa herufi hiyo.